Antoine Griezmann ana imani kwamba France ina nafasi kubwa ya kubeba kombe la michuano ya Euro mwaka huu ambayo inafanyika katika ardhi yao, lakini akisisitiza pia bahati inahitajika ili kufanya hivyo.
Mshambuliaji huyo wa Atletico Madrid anatajariwa kuwa moja ya silaha katika safu ya ushambuliaji chini ya kocha Didier Deschamps.
“Tuna wachezaji wakubwa ambao wanacheza kwenye timu kubwa, hivyo nadhani tuna kikosi chenye uwezo wa kubeba ndoo hii”,alisema Griezmann.
Lakini hata hivyo tunahitajika kuwa imara, tunapaswa kushinda michezo yetu yote mitatu ya mwanzo ili kuona nini kitatokea”.
“Tupo katika kundi zuri na timu yetu ipo katika maandalizi mazuri pia. Tunataniana sana katika vyumba vya kubadilishia nguo na sote tunapendana. Na unaweza kuthibitisha hilo uwanjani. Kila mmoja anatekeleza majukumu yake kwa asilimia 100. Kila mmoja ana msaada kwa mwenzake”.
Kuna wachezaji vijana na wenye uzoefu. Kuna Patrice Evra, Hugo Lloris..wachezaji kama hao wanaongea mambo mazuri sana katika vyumba vya kubadilishia nguo, vile vile tunao Kingsley Coman, Anthony Martial na Paul Pogba ambao kwa namna moja….labda niseme vichaa. Lakini tunafurahi sana kwa mambo yao.
Ufaransa ni moja ya mataifa yanayotazamwa kwa jicho la aina yake kutokana na kusheheni vipaji vingi hasa katika safu ya ushambuliaji, lakini Griezmann pia anaamini kuna mataifa kadhaa ya kuogopwa katika michuano hiyo.
Kuna Ujerumani, Uhispania na hata Italy pia. Sasa kwa hali hiyo lazima bahati pia ichukue nafasi yake.
Griezmann amekuwa na msimu mzuri akiwa na klabu yake ya Atletico baada ya msimu huu kuweka kimiani mabao 32 katika michuano yote.
“Kujiamini kunakuja kutokana na kufunga magoli na kucheza vizuri, mara nyingi nimekuwa nikijaribu kuhakikisha kuwa sipotezi mpira wangu wa kwanza”, alitanabaisha. “Kadri unavyozidi kugusa mpia ndivyo unavyozidi kufanikiwa katika kutoa pasi zako, na kuongeza kujiamini.
“Nimekuwa bora kwenye kila kitu, kulinda, kushambulia, mbinu, nguvu, shukrani kwa dhati kwa viongzoi, benchi la ufundi na wachezaji wenzangu, nimeimarika sana na naamini nitaendelea kuimarika zaidi katika uchezaji wangu”.
Griezmann pia aliongelea juu ya utofauti uliopo kati ya kocha wake wa klabu Diego Simeone na wa timu yake ya taifa Didier Deschmaps na kusema kwamba wana vitu kadhaa vinavyofanana.
“Kila mtu ana staili yake, sioni tatizo kwa kila mmoja, nawapenda wote”.
“Simeone anajitoa kwa kila kitu kwa ajili ya timu na Deschamps vivyo hivyo. Wote kwa pamoja ukizingua wanakukabili moja kwa moja na wote wanajua namna gani ya kuwapa confidence wachezaji kwa wakati muafaka”.
0 comments :
Post a Comment