Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa ili Tanzania iweze kuwa nchi ya viwanda, nishati ya uhakika inahitajika na kutaka makampuni kuwekeza katika uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi.
Profesa Muhongo ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika nyakati tofauti alipokutana na watendaji wa kampuni zinazojishughulisha na Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) lengo likiwa ni kupokea taarifa ya maendeleo ya miradi mbalimbali ya makampuni hayo ambayo yanafanya kazi kwa kushirikiana na Shirika la TPDC, British Gas (BG), Ophir, ExxonMobil na Statoil.
Profesa Muhongo amesema kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyopiga hatua kimaendeleo bila kuwa na nishati ya uhakika ya umeme na kuwataka wawekezaji kuchangamkia fursa kupitia gesi nyingi iliyogunduliwa.
Ametaja maeneo yanayohitaji uwekezaji katika kuzalisha umeme kwa kutumia gesi kuwa ni pamoja na Mtwara, Lindi, Somanga Fungu, na Mkuranga na kuongeza kuwa viwanda 37 vya umeme wa gesi pamoja na vya sementi vinahitaji gesi na kusisitiza kuwa iwapo sekta ya gesi itatumiwa ipasavyo inaweza kuchangia nchi kupiga hatua na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyosema.
Akizungumzia mikakati ya serikali katika kuzalisha wataalam katika masuala ya mafuta na gesi Profesa Muhongo amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa ufadhili kwa wanafunzi katika ngazi za shahada za uzamili na uzamivu katika vyuo vilivyopo nje ya nchi vyenye uzoefu katika fani hiyo, pamoja na uanzishwaji wa programu hizo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Madini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) Dk. James Mataragio amesema kuwa shirika hilo limekuwa likishirikiana na kampuni hizo katika hatua zote muhimu hususan katika kiwanda cha kuchakata gesi asilia kimiminika (Liquefied Natural Gas) na kuongeza kuwa mpaka sasa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda limeshapatikana.
Naye Meneja Mkazi wa Kampuni ya Statoil Tanzania, Øystein Michelsen, amesema kuwa kampuni yake ipo tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa miradi yake inakamilika kwa wakati ambapo kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na Serikali kwa kutoa ufadhili wa masomo katika masuala ya gesi na mafuta nje ya nchi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri.
Ameongeza kuwa kampuni ya Statoil imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriliamali kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara ili waweze kushiriki katika uchumi wa gesi kupitia utoaji wa huduma zake kwa Kampuni hiyo.
0 comments :
Post a Comment