Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekifungia kituo cha Radio 5 cha
mjini Arusha kinachomilikiwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
kwa kipindi cha miezi 3 pamoja na kuitoza faini ya shilingi milioni 5
huku kituo cha redio cha Magic FM, kikipewa onyo kali pamoja na kutakiwa
kuomba radhi kwa muda wa siku tatu mfululizo kwenye vipindi vyao vya
taarifa za habari.
Kwa mujiwa wa taarifa iliyosomwa na makamu mwenyekiti wa kamati ya
maudhui ya mamlaka hiyo, Joseph Mapunda, TCRA imetoa adhabu hizo kwa
kituo cha Radio 5 kutokana na kukiuka baadhi ya Kanuni za Huduma za
Utangazaji (maudhui) kupitia kipindi chake cha ‘Matukio’ kilichorushwa
Agosti 25, 2016.
“Maneno ya Lema yalilenga kuhamasisha wananchi kupambana na jeshi la
polisi na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa
taifa,” alisema Mapunda.
“Baada ya kusikiliza maelezo ya utetezi kamati imeridhia kuwa kipindi
cha matukio kilikiuka baadhi ya kanuni za maudhui namba 5(a,b,c,d,f,h)
6(2) (b, c) na 18 (1) (b),” ameongeza.
Makamu huyo ameendelea kwa kusema kuwa adhabu hiyo ya faini
iliyotolewa kwa kituo hicho cha redio inatakiwa kulipwa ndani ya siku 30
kuanzia leo lakini pia kama watataka kukata rufaa nafasi hiyo ipo wazi
kwa muda wa mwezi mmoja.
Akiongelea kuhusu adhabu waliyoitoa kwa kituo cha redio cha Magic FM,
Mapunda alisema, “Baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya
utetezi yaliyotolewa na uongozi wa Magic FM, kamati imeridhika kuwa
kipindi cha ‘Morning Magic’ kilikiuka baadhi ya kanuni za huduma za
utangazaji ya mwaka 2005. Kamati ya maudhui inaamua kutoa onyo kali kwa
Magic Radio.”
“Pia wanatakiwa kumuomba radhi Rais John Magufuli, wasikilizaji na
wananchi kwa ujumla. Tangazo la kuomba radhi litolewe kwa siku tatu
mfululizo katika taarifa za habari za saa 10.00 alasiri, na 3.00 usiku
kuanzia tarehe 17,9,2016.”
0 comments :
Post a Comment