Wanafunzi wa kike nchini wametakiwa kuongeza bidii katika masomo ya
sayansi, ili waweze kulisaidia taifa katika sekta mbalimbali muhimu ikiwemo
sekta ya afya.
Kauli hiyo imetolewa na naibu waziri wa elimu, sayansi na teknolojia
Mhandisi Stella Manyanya, wakati wa mahafali ya nne ya shule ya sekondari ya Wama Nakayama, iliyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Aidha Manyanya ameeleza kuwa wanafunzi wanatakiwa kuangalia upungufu uliopo
kwenye sekta mbalimbali nchini huku akikazia sekta ya afya ambayo amesema bado
ina changamoto ya uhaba wa wafanyakazi na kuwahimiza wanafunzi hao kutokata
tamaa ya masomo hayo kwani ndio yenye uhakika wa ajira.
Manyanya amesema kuwa ili kuepusha hatari mbalimbali zinazotokea kwenye
vituo vya afya ikiwemo vifo vya akina mama, inahitajika nguvu ya uwepo wa
wataalamu wa kutosha wa afya kwenye sekta hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa shule hiyo ambaye ni mke wa rais mstaafu wa
Tanzania Dkt Jakaya Kikwete, Mama
Salma Kikwete, amesema kuwa anajivunia maendeleo mazuri ya shule hiyo na
kuwataka wanafunzi waendelee kujifunza zaidi yale wanayofundishwa shuleni hapo.
Kwa upande wa nidhamu, Mama Salma
Kikwete amesema anawashukuru wanafunzi wa shule hiyo kwa kuwa na nidhamu
nzuri huku akisisitiza kuzidi kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuwapotosha.
Wama Nakayama ni shule iliyoanzishwa mwaka 2010 na imetokana na majina
mawili ya Wama na Nakayama ambapo Wama inasimama kama taasisi ya wanawake na
maendeleo, Nakayama inasimama kama jina la mdau wa kwanza wa shule hiyo
kuisaidia kimaendeleo, ambaye ni mfanyabiashara mkubwa kutoka nchini Japan.
0 comments :
Post a Comment