Serikali imesema bado inadaiwa na walimu deni linalofikia Sh67.3 bilioni, ikiwamo mishahara.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jaffo alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Aida
Khenani bungeni.
Khenani bungeni.
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua Serikali imechukua hatua gani kumaliza madai ya walimu ya muda mrefu nchini.
Pia, alihoji kuhusu madai ya walimu waliosahihisha mitihani ya kidato cha nne mwaka jana ambao hawajalipwa hadi sasa.
Naibu Waziri huyo alisema Serikali imeendelea kulipa madeni ya walimu kupitia mamlaka zake kila yanapojitokeza.
“Mfano, Oktoba 2015, Serikali ililipa Sh20.1 bilioni na Februari mwaka huu imelipa Sh1.17 bilioni za madeni ya walimu nchi nzima,” alisema Jaffo.
Alitoa mchanganuo kuwa kati ya kiasi kinachodaiwa, alisema Sh17.5 bilioni ni madeni yasiyo ya mishahara wakati madeni ya mishahara yanafikia Sh49.8 bilioni ambayo kwa pamoja yanafanyiwa uhakiki.
Kuhusu malipo ya walimu waliofanya kazi ya kusahihisha mitihani alisema baadhi ya mikoa haijapeleka madai yao hadi sasa licha ya kuwa mwisho wa kupelekwa ilikuwa ni Aprili 15.
Alisema mikoa tisa tu ndiyo ilipeleka na kuitaja kuwa ni Mbeya, Mara, Tanga, Arusha, Kigoma, Lindi, Mtwara, Kilimanjaro na Iringa.
Alisema madeni hayo ya mikoa hiyo yanahakikiwa ili walimu walipwe.
0 comments :
Post a Comment