Yanga imerejea kileleni mwa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara baada ya kuifunga mtibwa Sugar kwa goli 1-0 kwenye mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa taifa. Yanga ilienguliwa kileleni mwa ligi na mahasimu wao Simba takribani
mwezi mmoja ulipita lakini wamerejea kwenye nafasi yao kufuatia kushinda mechi zao za viporo.Bao pekee la ushindi limefungwa na Simon Msuva dakika ya 48 kipindi cha pili kwa kiki ya chinichini aliyoiachia akiwa nje ya eneo la hatari na kumshinda mlinda mlango wa Mtibwa Sugar Said Mohamed.
Licha ya kupata ushindi huo, Yanga ilipoteza nafasi nyingi za kupata magoli mengi zaidi kutokana na ubora wa golikipa Said Mohamed ambeye leo alikuwa kwenye kiwango bora na kuokoa michomo kadhaa ya washambuliaji wa Yanga.
Ushindi wa Yanga dhidi ya Mtibwa unaifanya timu hiyo kufikisha pointi 59 na kukaa kileleni mwa ligi kwa pointi 2 zaidi ya Simba ambayo inashuka hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi zake 57 lakini timu hizo zikiwa zimecheza mechi 24.
Yanga imeishinda Mtibwa Sugar katika game zote mbili za ligi kwa mara ya kwanza baada ya kufanya hivyo kwa mara ya mwisho msimu wa 2008/09.
Yanga imeifunga Mtibwa jumla ya magoli matatu msimu huu na kuondoka na pointi zote sita baada ya michezo miwili.
Simon Msuva ameifungia Yanga magoli mawili katika mechi mbili mfululizo. Alifunga goli la kwanza kwenye mchezo wa Yanga vs Mwadui Jumatano walipopata ushindi wa magoli 2-1 lakini mchezo dhidi ya Mtibwa amefunga goli pekee.
0 comments :
Post a Comment