Mshumaa umeteketeza bidhaa za maduka 7!


Misungwi. Mshumaa ulioachwa ukiwaka katika moja ya vibanda vya eneo la Njiapanda ya Usagara, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, umesababisha  hasara ya mamilioni ya fedha baada ya maduka saba yenye bidhaa mbalimbali kuteketea usiku wa kuamkia Julai 11.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Deogratias Madata amesema moto huo ulianza saa mbili usiku na kuenea katika maduka mengine, kabla ya kudhibitiwa na wananchi waliokuwa wakisaidiana na askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza.
“Moto huo ulianza katika kibanda ambacho hakijaunganishwa na huduma ya umeme, ambacho siku zote mmiliki wake anatumia mshumaa. Inawezekana alijisahau kuzima wakati anafunga biashara usiku,” amesema Madata.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Mussa Kaboni alisema walifika eneo la tukio dakika 20 baada ya kupata taarifa.
Kaboni amesema umbali wa kutoka Mwanza mjini hadi Usagara ambao ni takriban kilomita 20, ulisaidia askari kufika eneo la tukio mapema na kufanikiwa kuudhibiti moto huo.
“Kama wamiliki wa maduka yale wangekuwa na vifaa vya dharura vya kuzima moto, madhara yangekuwa kidogo kuliko ilivyotokea,” amesema Kaboni.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Usagara, Zubeir Kilala amesema moto huo ulifanikiwa kudhibitiwa kutokana na ushirikiano kati ya wananchi na askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji. 
Chanzo: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment