Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kumeripotiwa ongezeko la wanafunzi laki sita waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza tangu serikali yake ''kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari''.
Rais Magufuli aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa ugavi wa madawati yanayotengenezwa kutokana na fedha zilizopatikana baada ya bunge kubana matumizi katika bajeti yake katika uwanja wa Karimjee Jijini Dar es salaam.
Kiongozi huyo alisema kuwa idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5.
''Hali hiyo ilisababisha upungufu wa madawati 1,400,000 lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa ambapo mpaka sasa zaidi ya madawati 1,000,000 yametengenezwa'' taarifa hiyo ya kaimu mkurugenzi wa mawasiliano ikulu Gerson Msigwa ilieleza.
Madawati 61,385 ambayo yametengenezwa katika awamu ya kwanza na yatafuatiwa na madawati mengine 60,000 yatakayogawiwa katika awamu ya pili na yote kwa ujumla yatagharimu shilingi bilioni 4
Mikoa itakayonufaika katika awamu ya kwanza ya ugawaji wa madawati hayo ni Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.
Aidha, Dkt. Magufuli amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza kuongeza kasi katika utengenezaji wa madawati ili yakamilike haraka na kuanza kutumika.
Chanzo: BbcSwahili
0 comments :
Post a Comment